TANGAZO LA UDHAMINI WA ELIMU YA JUU KWA MWAKA 2017/18
Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere unaosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), unatangaza kutoa nafasi za udhamini (scholarships) kwa masomo ya elimu ya juu kwa mwaka 2017/18.
Ufadhili huu, unalenga kuongeza hamasa na ufaulu kwa wanafunzi wa kike hapa nchini katika masomo ya Hisabati na Sayansi. Unajumuisha gharama zote za ada, pesa za kujikimu, mafunzo ya vitendo na vifaa vya kujifunzia ikiwemo kompyuta mpakato (Laptop).
Ufadhili huo utatolewa kwa wanafunzi raia wa Tanzania wenye ufaulu wa kiwango cha juu waliosajiliwa vyuo vikuu vinavyotambulika nchini.
Kwa shahada ya kwanza, ufadhili utatolewa kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu- yaani daraja la kwanza miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa wa kidato cha sita mwaka 2017, kwa masomo ya Hisabati na Sayansi kwa wanafunzi wa kike tu na masomo ya Uchumi, TEHAMA, Uhasibu na Fedha kwa wanafunzi wa kike na wa kiume.
Kwa upande wa shahada ya uzamili, ufadhili utatolewa kwa wanafunzi wa kike na wa kiume waliofaulu kwa kiwango cha juu katika shahada ya kwanza kwa kozi za Hisabati, Sayansi, Uchumi, TEHAMA, Uhasibu na Fedha.
Tangu kuanza ufadhili huo mwaka 2013/14 hadi hivi sasa (2016/17), jumla ya wanafunzi wa Kitanzania Ishirini na Nane (28) wamepata Ufadhili huo; kati yao Ishirini (20) ni wanawake na Nane (8) ni wanaume.
Baadhi yao wamekwishamaliza kozi zao na wengine wanaendelea na masomo yao katika fani za Uhandisi-Mafuta na Gesi, Sayansi ya Mafuta na Jiolojia, Sayansi – Hisabati, Sayansi Uhandisi Ujenzi, Udaktari, Ufamasia, Usanifu Majengo, Sayansi (Kemia), Sayansi – Uchambuzi wa Masuala ya Bima (actuarial sciences), Uhasibu, Fedha, Uchumi na Takwimu, TEHAMA na Uongozi; katika vyuo vikuu mbalimbali vinavyotambulika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mfuko unawahimiza wanafunzi wote, hasa wa kike, katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujibidisha katika masomo na kupata ufaulu wa juu. Kwa Shahada ya Kwanza orodha ya wanafunzi kumi (10) bora wa kidato cha sita 2017 itaombwa toka Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) baada ya
matokeo kutoka. Kwa Shahada ya Uzamili, maombi yatakaribishwa rasmi kuanzia mwezi wa sita, 2017.
Fomu za Maombi kwaajili ya Udhamini huu zitapatikana katika Tovuti ya Benki Kuu, ofisi za Benki makao makuu na matawini kuanzia mwezi wa sita, 2017.
Limetolewa na:
Mwenyekiti,
Kamati ya Mfuko wa Udhamini wa
Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere,
Benki Kuu ya Tanzania,
2 Mtaa wa Mirambo,
11884, DAR ES SALAAM.
Post a Comment